ITIFAKI IMEZINGATIWA
ITIFAKI IMEZINGATIWA! NDIYO KITU GANI HASA?
Jumamosi tarehe 26 Juni, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Ijumaa tarehe 25 Juni, 2021 alikutana na Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Wakatoliki (TEC) Kurasini Dar es Salaam na kuhutubia taifa kutokea hapo.
Nilipata bahati ya kufuatilia mkutano ule na miongoni mwa mambo ambayo yalikamata kichwa changu ni hili neno "ITIFAKI IMEZINGATIWA."
Nimekuwa nikijiuliza mara kwa mara, ni nini hasa? Lina maana gani hasa?
Nilichobaini katika mkutano ule ni kwamba, tukiacha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye itifaki ni sehemu ya maisha yake, mtu mwingine pekee anayeifahamu itifaki vilivyo ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga.
Baba Askofu Nyaisonga anaijua itifaki ya Kanisa Katoliki na ya nchi mpaka unasikia raha kumsikiliza. Wengine wote waliobaki niseme tu wana changamoto katika kujua itifaki ni nini hasa?
Na si katika mkutano ule Maaskofu tu, niliwahi kueleza kosa lililofanyika katika tukio moja la dini ya kiislamu kwenye mashindano ya Quran ambapo baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kutoa hotuba kikanuni haikupaswa mtu mwingine kutoa hotuba labda Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi angetoa ruhusa lakini ajabu kiongozi mmoja wa dini alianza kuzungumza tena.
Wabunge na wanasiasa kwa ujumla huwa wanajisikia raha sana kusema, 'ITIFAKI IMEZINGATIWA' jambo ambalo si sahihi.
Kwa ufupi ni hivi; 'Itifaki ni Kanuni zinazoongoza matukio rasmi ya kitaifa ama kimataifa'.
Kanuni hizi ni utamaduni wa kimataifa ambao umekubalika na unatabirika ukiwa na lengo kuu la kumfanya kila aliyehudhuria tukio kujisikia amethaminiwa na kuheshimiwa na mwenye amani moyoni.
Kanuni hizi zinaongoza utaratibu wa namna ya viongozi wakuu kuingia, kutoka, kukaa na hata kutambulisha na kutambulishwa.
Kwa mfano; katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuna viongozi wa Kitaifa wanane ambao ni:
(1) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(2) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(3) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
(4) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(5) Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
(6) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
(7) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(8) Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kunapokuwa na tukio la kitaifa na wakawepo wote, 'mzungumzaji atapaswa kuwataja hawa wote kwa majina yao yote kwa usahihi wake na vyeo vyao.'
Pale wanapokaa viongozi hawa huwa tunaita 'meza kuu'
Baada ya hapo mzungumzaji atawataja walio katika 'jukwaa kuu' kwa ujumla wao wote kwa mfano, 'waheshimiwa mawaziri mbalimbali wa Serikali zetu mbili, waheshimiwa wabunge, waheshimiwa wakuu wa mikoa, waheshimiwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama n.k na wageni wote wengine waliopo kwa mujibu wa msemaji alivyoandikiwa.'
Baada ya kutaja mtiririko huo mzungumzaji atamalizia, 'wageni mashuhuru mliopo hapa, wageni waalikwa (kama wapo) mabibi na mabwana, nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.'
Hii ndiyo itifaki ya salamu, na siyo ile tuliyojizoesha wengi mzungumzaji anaenda kwenye maiki na kutaja watu wawili kisha anasema 'Itifaki Imezingatiwa. IPI?'
Tujiuulize, kusema itifaki imezingatiwa bila kufuata kanuni inavyotaka ndiko kutawafanya ambao hawakutajwa kuona kuwa wamethaminiwa na kuheshimiwa?
Au tujiulize, kwa mfano mtu amewekewa chakula, kikanuni hasa kwa sisi watanzania tunamtarajia huyo mtu aanze kunawa kabla ya kula. Hivi mtu huyo akila bila ya kunawa ikisha akatuambia nimezingatia kanuni ya kula (wakati tumeona hajanawa), ni sahihi?
Kimsingi kanuni inataka uwataje wale wote waliopo katika orodha ambayo muhusika unakuwa umepewa mpaka kuishia kwenye salamu hiyo ndiyo itifaki na si kusema itifaki imezingatiwa.
Hili neno (itifaki imezingatiwa) halipo duniani popote na halipaswi kutamkwa labda sijui sisi waafrika tunalipendea nini?
Nilipata kukutana na mgeni fulani kutoka nchi za Ulaya aliniambia sisi waafrika tunapenda kutaja hilo neno (itifaki imezingatiwa) kwa sababu ni wavivu wa kufuata kanuni. Nilikwazika kwa maneno yake lakini naona ni sisi wenyewe tunawathibitishia wanaojua itifaki huo uvivu.
Ushauri wangu ni huu, 'hakuna neno itifaki imezingatiwa kinachopaswa kufanya ni kutaja mtiririko kwa mujibu wa ulivyopangwa na kumalizia na salamu bila ya kutaja hilo neno.'
Ushauri wangu wa ziada ni kuwa Wabunge, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala na watendaji wengine wapatiwe kozi hizi za itifaki ili waweze kuenenda vizuri katika majukumu yao.
Chuo cha Diplomasia kina jukumu hilo la kufundisha masuala hayo, si vibaya Serikali na hata Sekta binafsi ikalitazama hili kwa kuwapitisha kwenye taaluma hiyo.
Comments
Post a Comment