UMUHIMU WA KUTUNZA MUDA

*UMUHIMU WA KUTUNZA MUDA*

Na SS Nyakubandya

Ni kawaida ya mswahili kusikia akisema *"napoteza poteza muda*".

Wachina wanamsemo:"inch ya muda ni sawa na inch ya dhahabu lakini huwezi kununua inch ya muda kwa inch ya dhahabu"

Muda ni mfinyu sana na kila jambo limeegemezwa katika muda, matumizi yako mazuri ya muda yatakufanya upate unachokitaka katika hii dunia na kesho akhera.Ikiwa siku moja ina masaa 24, swali ni je haya masaa 24 unayatumiaje? Wote waliofanikiwa wametumia masaa haya haya 24 ambayo kila mtu anayo. Kwa bahati mbaya muda unasifa ambazo hakuna mtu angependa kuzisikia; muda uko kasi sana kuliko chochote, muda ndiyo kitu pekee ambacho hakiwezi kufidiwa katika maisha lakini pia ndio kitu pekee kisichoweza kusimama.(Tizama masaa yako na mambo unayoyafanya ndani ya saa 24)

Mambo yanayopoteza muda ni mengi sana ila hapa nitataja machache ikiwemo kutizama *mpira* (mashabiki naomba mnisamehe hapa maana najua hamtaki kusikia jambo hili) ndani ya lisaa limoja na nusu unaweza kusoma kitabu ukapata maarifa ya kukusaidia kitu fulani, ndani ya muda wa lisaa na nusu unaweza kuhifadhi chochote katika Qur'an na pia unaweza kufanya shughuli ya uzalishaji au kuhudhuria semina na ukapata jambo la kukusaidia wewe na wengine kwa kutumia kiingilio hicho hicho unacholipia uwanjani. Mbili *kutizama filamu*, tatu ni kupiga *soga vijiweni* na kutokuwa na ratiba ya siku ambayo inakuwa ndio dira yako ya siku. Ni rahisi sana kwa mtu kukuharibia ratiba yako na kumtekelezea yake. Nne ni *usingizi* na hasa kwa kwa dada zangu:kuna hii dhana ya masaa 8:Masaa 8 ni lazima kwa mama mjamzito kwaajili yake na ukuaji wa mtoto na watoto wadogo ambao wao wanaweza kulala hadi masaa 12 kwa siku ila sio lazima kwa kila mtu. Mtu mzima anahitaji masaa yasiyopungua 5-6  yanatosha sana kwa siku.Inawezekana kutengeneza tabia ndani ya mwezi moja ikawa imetengenezeka na hii ndio maana ya falsafa ya funga ya mwezi ramadhani yaani tabia iliyojengeka ndani ya mwezi mmoja inaweza kuwa tabia ya maisha yako.Siku moja sayyidina Omar ibn Khattab(ra) aliuliza *"Ni lini nitalala? Ikiwa nitalala usiku nitashindwa kutekeleza wajibu wangu kwa mola wangu, nikilala mchana nitashindwa kutekeleza wajibu wangu kwa watu wangu*. Haya wewe una nini hadi ulale masaa 8-12 kwa siku,hao wanaosema ulale masaa nane wao wenyewe hawalali masaa hayo. (Tengeneza ratiba ya mambo ambayo lazima uyafanye kila siku)

Tafiti zinaonesha *Koala* ndiye mnyama anaelala masaa mengi kuliko mnyama mwingine yoyote, ulala masaa 20-22 na hutumia masaa 2 hadi 4 kwaajili ya kutafuta chakula na kisha urejea mtini kuuchapa tena usingizi, tusiishi maisha ya koala ya kula, unalala kisha mauti bila kufanya jambo kubwa katika maisha ambalo ni rejea katika jamii. (Punguza masaa ya kulala kisha yape jukumu tija utaona manufaa yake)

Miongoni mwa waja wema waliotumia muda vyema ni pamoja na imamu Nawawi ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 40. Alipofikisha miaka 25 alianza kuandika na alijaaliwa kuandika vitabu 50 ndani ya miaka 15 jambo lililomfanya kutingwa sana na kukosa hadi muda wa kuoa. (Imamu Nawawi alikosa muda wa koa kwa kiswahili rahisi ni kuwa muda ulimpungua, wewe unapata wapi ujasiri wa kupoteza muda) *"Wanaotumia muda vyema, dunia inawakumbuka na wanamarejeo mazuri  kwa mola wao"*  Jiulize, ikiwa mauti yamekukuta sasa nini umetanguliza na nini umeacha kama urithi wa dunia au ndiyo utakumbukwa na familia yako tu) Shaaban Robert katika kitabu chake cha *"maisha yangu na baada ya miaka 50"* anasema: Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa  duniani. Imam Nawawi ni Miongoni mwa waja wema wenye majina mazuri duniani,  vip mimi na wewe.

kati ya changamoto kubwa ni pale unapofanya maamuzi ya kuwa mtunza muda; unaweza kupewa majina mengi sana, unaweza kugombana na watu, usikate tamaa tabia nzuri inahitaji subra katika kuijenga, mwisho watazoea na wewe utakuwa rejea yao na uenda ukaisaidia jamii kwa uamuzi wako huo wa kuanza kutunza muda.(Jambo jema halihitaji watu wengi kulifanya au kulianzisha)

Kumbuka kanuni ya Allah inasema *"Hakika mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao 13:11"*


*"Tunza muda ukutunze"* 

Tunakumbushana

Comments

Popular posts from this blog

SHULE ZENYE ADA KUBWA ZAIDI TANZANIA

STOP SHARING

RAFIKI WA KWELI