NITAOA NIKIFIKA THELATHINI
NITAOA NIKIFIKA THELATHINI
Si kama nataka kufa, kwa haya nitokwambia
Ila nofia kujuta, pindi yakikutokea
Nogopa nafsi nisuta, mjomba nsipokwambia
Nitaoa nikifika thelathini
Natambua nia yako, nia unopigania
Sikukwacha peke yako, pekee kiteketea
Shikamana na wenzako, usia me nakwambia
Nitaoa nikifika thelathini.
Nataka kupa wosia, li kazi uufanyie
Sio uje puuzia, sitajilaumu mie
Kidogo hebu sikia, kisha ukazingatie
Nitaoa nikifika thelathini.
Wangindo mi nawajua, na hasa nawatambua
Kidogo kifanikiwa, haraka taka kuoa
Mjomba we zingatia, usi harakie ndoa
Nitaoa nikifika thelathini.
Kama ukipata kazi, tulia kwa kujipanga
Usijivishe li vazi, kabla maisha kujenga
Tena ipo wazi wazi, kuoa ni kujifunga
Nitaoa nikifika thelathini.
Misingi ikisimama, hapa hakuna utata
Usimuulize mama, ila shauri we kata
Kuoa ni jambo jema, ila maisha kipata
Nitaoa nikifika thelathini.
Tena sipende umimi, ukoo kuurithia
Yako yaweke moyoni, na mengine puuzia
Hutobaki masikini, labda apende jalia
Nitaoa nikifika thelathini.
Ukioa thelathini, si kwamba umechelewa
Iweke tu akilini, watoto taka lelewa
Mke utampa nini, kama hujajaaliwa
Nitaoa nikifika thelathini.
Nataka kusema mengi, ila utapuuzia
Ukayatoa msingi, kwa mbali kuyatupia
Mke anataka mengi, mjomba we zingatia
. .nitaoa nikifika thelathini.
BAHARI/ Kibwagizo/ kiitikio:
Sijui niseme nini, kama sio mesikia
Nitaweka akilini, le yote lo niambia
Nitaoa thelathini, mjomba mi nakwambia
Nitaoa nikijipanga
Nitaoa nikijenga
Nitaoa nikipenda
Nitaoa nikifika thelathini
Comments
Post a Comment